Mara baada ya kukufndisha juu ya FUNGUO TANO za kufungua malango na milango, sasa nataka nikufundishe juu ya kipengele kingine ambacho ni ;
SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;
Maombi yetu ya
Kufungua Milango na Malango yaliyofungwa inahitaji Uhodari na Uthabiti katika
Imani, hivyo lazima silaha hizi zitumike ndipo Milango na Malango yaliyofungwa
yatafunguliwa. Kufungua kilichofungwa si kazi rahisi. Maandiko matakatifu
yanasema; “Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani; kwa maana
kushindana kwetu si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka juu ya
wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa Roho, kwa
sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kushindana siku ya uovu,
na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” Waefeso 6:10-14
Maisha yetu ya
Kristo yapo katika mgongano wa kiroho na shetani na huu mgongano unaitwa VITA
VYA IMANI. Ambavyo vinaendelea hadi atakapokuja mara ya pili Yesu Kristo
kuvikomesha. Lakini ushindi wa mtu wa Mungu umehakikishwa na Kristo mwenyewe
kwa njia ya kifo chake pale msalabani. Alipokufa na kufufuka ametangaza ushindi
kwa kila amwaminiye tangu wakati ule hata sasa tunashinda na zaidi ya kushinda.
Palipo na neno “KUSHINDA” maana yake pana neno “KUSHINDANA”.
Maisha yetu ya
imani ni ya kushindana na kushinda. Wengine kwa kutokujua, adui alipokuja
kushindana nao wakaogopa, wakaona Mungu amewaacha na kujiuliza maswali mengi
KWANINI BWANA AMEYARUHUSU HAYA? Kumbe maisha ya ukristo halisi ni vita sio
lelemama ndiyo maana BWANA anasema tuwe hodari na moyo wa ushujaa. “Uwe
hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakaye warithisha watu hawa… uwe
hodari tuu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote… usiache
kwenda mkono wa kuume au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.”
Yoshua 1:6-7
BWANA umtumia
mtu hodari na mwenye moyo wa ujasiri sio mtu legelege na dhaifu. Ndiyo maana
alimtumia Daudi kumpiga Goliati kwa sababu alikuwa na moyo wa uhodari na
ujasiri mwingi. Daudi hakwenda vitani kubahatisha bali alikwenda ksuhindana na
kushinda ndivyo ilivyotokea. Maandiko yanasema; “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga
silaha zake alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama lakini mtu mwenye nguvu
kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote
alizokuwa akizitegemea na kuyagawanya mateka yake.” Luka 11:21-22
Yesu Kristo
anahimiza kujifunga silaha zetu na kuyalinda Malango na Milango yetu. Pasipo
kujifunga silaha hatuwezi kumshinda yule adui shetani. Lazima uzivae hizi
silaha ndipo zitakazofanya Ushinde Falme za giza, Wakuu wa giza hili na
kuyashinda Majeshi ya pepo wabaya. Maandiko yanasema; “Maana ingawa tunaenenda katika
mwili hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili
bali zinauwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.” 2Wakorinto 10:3-4
Vita vyetu vya
kiroho sharti vipiganwe kwa silaha za rohoni – pasipo kuvaa hizi silaha za
kiroho hatuwezi kuziangusha ngome zilizojengwa kinyume na zenye kuhakikisha
Malango hayafunguliwi.
SILAHA
YA KWANZA
Zipo silaha nane za kiimani zenye nguvu za kufungua malango na
milango iliyofungwa katika maisha yetu ya kiroho na kimwili. Silaha hizo ni:-
(i)
KATAA
Imani ni kuwa na hakika katika Mungu na
mwenye haki ataishi kwa imani. Maandiko matakatifu yanaonyesha waziwazi ya kuwa
msingi wa wokovu ni imani. Yatupasa kuyakataa yale tusiyoyaamini katika imani
yetu, mfano wa Musa alivyokataa kuitwa mtoto wa binti Farao, japo kuitwa mtoto
wa binti Farao kulikuwa na faida nyingi za kimwili lakini akachagua ufalme wa
Mungu na haki yake kuliko ufalme wa Farao ambao mwisho wake ni kutupwa jehanamu
ya moto. Hivyo Musa akatumia silaha hii ya kwanza ya KUKATAA matokeo yake BWANA
akamtumia kama shujaa na mkombozi wa wana wa Israeli toka utumwani Misri.
Maandiko matakatifu yanathibitisha; “Kwa Imani Musa alipozaliwa alifichwa miezi
mitatu na wazazi wake kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri wala hawakuogopa
amri ya mfalme KWA IMANI MUSA
ALIPOKUWA MTU MZIMA ALIKATAA KUITWA MWANA WA BINTI FARAO. Akaona afadhali
kupata mateso kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo akihesabu
kushutumiwa kwake Kristo ni UTAJIRI MKUU kuliko hazina za Misri kwa kuwa
aliyatazamia hayo malipo. Kwa Imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme,
maana alistahimili kama amuonaye yeye asiyeonekana kwa Imani alifanya Pasaka,
na kule kunyunyiza damu ili yule mwenye kuangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse
wao” Waebrania 11:23-28
Musa alikataa kuitwa mtoto wa binti
Farao, ukawa ndio mlango wa ukombozi wa wana wa Israel kutoka katika milango ya
kuzimu ya Farao. Hii ni silaha kubwa sana ambayo lazima tuivae kabla ya mambo
yote. Ni lazima kwa Moyo wako wote na Roho yako yote na kwa Akili zako zote Kataa hali uliyonayo
katika ulimwengu wa Roho ama katika Mwili. Maandiko matakatifu yanasema; “Tumbo
la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti
na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”
Mithali 18:20-21
Ukiri katika
ulimi una nguvu ya kuangusha malango na milango ya kuzimu hivyo ulimi wa imani
ni mti wa uzima. Ni vema kutumia ndimi zetu kujitamkia mema sisi wenyewe,
kutamka mema kwa watoto wetu na juu ya mali zetu maana BWANA Mungu alitamka iwe
na ikawa. “Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai
kitu” Mithali 10:20
Dada
mmoja pale Morogoro eneo la Forest aliokoka akiwa na miaka kumi na mitano
(Miaka 15), siku moja akiwa anatoka shule pale Morogoro mjini, alikutana na
mvulana mmoja kumbe ni mjumbe wa shetani (mtu jini) lakini yeye aliona ni
mvulana, wakasalimiana, lakini kumbe huyu binti amevamiwa na nguvu za yule
jinni kwa sababu alimwambia dada nimekupenda naye akasema asante kama utani
lakini ndo ukiri wa kinywa. Baada ya hapo huyu binti alianza kuota ndoto mbaya,
anafanya mapenzi; hiyo hali iliendelea kwa muda mrefu akiwa ndani ya wokovu.
Huyu binti alipokuwa anakuja kwangu kuniona alikuwa na umri wa miaka thelathini
na sita (Miaka 36) akiwa bado hajaolewa, hiyo ilikuwa mwaka 2012, akisema;“Mchungaji
nimefunga na kuomba na nimetoa sadaka sana lakini sipati mpenyo, ee Mtu wa
Mungu niombee.”
Wakati naanza
kumpa ushauri ili nipate kumwombea, nikaitiisha ile nguvu iliyo mfunga
kwa jina lenye nguvu la Yesu Kristo. Ndipo nguvu ya pepo jinni dume likapiga
kelele likidai huyu binti ni mke wake, limemuoa akiwa na umri wa miaka kumi na
mitano kule Morogoro. Nikaipinga ile nguvu ya pepo, nikasema huyu ameokoka,
ninyi mnawezaje kukaa ndani yake? Nikahoji
tena ni mlango gani mliotumia
kumfunga huyu binti; yule jini akasema waziwazi huyu binti ni mvumilivu na
mwaminifu sana kwa huyo Mungu wenu, lakini mimi ninammiliki kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kunikataa na
kuitengua ndoa yetu, kwani hujui imeandikwaje katika Warumi? “Kwasababu
ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya
kuwa Mungu alimfufua katika wafu, Utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata
kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Warumi 10:9-10
Yule kijana
(Jini) alimwambia binti nakupenda naye akakubali lakini hawakuonana tena na ni
miaka zaidi ya kumi na sita ndoa ipo katika ulimwengu wa roho. Ukiri una nguvu
ya Uzima ama Mauti. Ni lazima ukatae na
utengue kila mkataba na maagano yote ya giza sawasawa na kuamini kwako. Ndiyo
maana Musa alikataa kwanza kabla ya wito wake. Tendo la kukataa kuitwa binti
Farao ndilo likamfanya Mungu amuite kwa kazi yake.
Wakristo wengi
wanataka kufunguliwa Milango na Malango lakini bado hawajakataa kabisa Mizimu
ya ukoo, Mizimu ya mababu na mabibi zao, maagano mbalimbali walioungamanishwa
kwayo kabla ya wokovu. Usikiri
Udhaifu juu yako, juu ya watoto wako, juu ya mume wako, juu ya mke wako, juu ya
kazi yako, juu ya ndoa yako wala juu ya maisha yako.
“Neno BWANA lilinijia, kusema, kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua,
na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; Nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.
Ndipo niliposema, Aa, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.
LAKINI BWANA akaniambia, USISEME, Mimi ni mtoto maana utakwenda kwa kila
nitakayekutuma kwake, nawe UTASEMA KILA NENO NITAKALOKUAMURU. Usiogope
kwasababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana” Yeremia 1:4-8
Usiseme kinyume na Neno la Mungu juu yako maana BWANA anakuwazia mema naye
ulituma Neno kwako lipate kukuponya na kukufungulia milango na malango ya
Baraka na Ustawi.
Angalia Musa
pamoja na BWANA kumtumia katika kutenda maajabu na miujiza mingi, lakini Musa
alikufa akiwa na utasi (kigugumizi) kwa
sababu hakuukataa udhaifu huo bali aliukubali kuwa sehemu ya maisha yake.
Maandiko yanathibitisha;
“Musa
akamwambia BWANA, Ee Bwana, mimi si msemaji tokea zamani, wala tokea hapo
uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni
mzito. Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani
afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi,
BWANA? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha
utakalolinena. Akasema, Ee Bwana nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo
utakayemtuma. HASIRA YA BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, je! Hayuko
Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na
hayo, tazama, anakuja kukulaki, naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe
utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa
chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa
msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa
mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo
utazifanya zile ishara.” Kutoka
4:10-17
Mungu
alimkasirikia Musa kwa kitendo cha kukataa Uponyaji wa kinywa chake. Matokeo
yake mtumishi wa Mungu Musa mpaka anakufa, alikufa akiwa na utasi (kigugumizi).
Pia tunajifunza kwa YABESI; alikataa maisha
ya huzuni, Bwana akageuza huzuni zake kuwa heshima. Kabla ya kupokea hicho
unachotaka lazima uvae Silaha hii ya kukataa utaona mlango unafunguka
mbele yako.“Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze, na mamaye akamwita
jina lake Yabesi, akasema, Ni kwasababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi
akamlingana Mungu wa Israeli, akasema, Lau kwamba ungenibarikia kwelikweli, na
kunizidishia hozi yangu na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na
uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu!
Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.” 1Nyakati 4:9-11
Pamoja na jina
lake kuitwa huzuni, Yabesi alipomjua Mungu alikataa kuitwa huzuni, akakataa
maisha ya huzuni. Ndani mwa Maombi haya ya Kufungua Milango na Malango ni
lazima tukatae malango yote yaliyotupwa juu yetu au tumezaliwa nayo, maana katika ukiri wa Imani mna nguvu ya
kufungua Milango na Malango.
Tunajifunza kwa AYUBU; Pamoja na
mateso ya zaidi ya miaka kumi na saba (miaka 17), Kuugua, Kufilisika na Misiba,
lakini bado mtumishi huyu wa Mungu alikataa
kutamka kinyume cha Imani yake katika Mungu. Katika mambo yote Ayubu
hakufanya dhambi wala kumuwazia Mungu kwa upumbavu. “Lakini mimi najua ya kuwa
Mteteaji wangu yu hai, Na yakuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi. Lakini,
pasipokua na mwili wangu nitamuona Mungu; Nami nitamuona mimi nafsi yangu, Na
macho yangu yatamtazama, wala si mwingine, Mtima wangu unazimia ndani yangu.”
Ayubu 19:25-27
Haya maneno
yalifungua Mlango na Milango ya Ayubu tena akainuliwa toka kwenye shimo la uharibifu. Baada ya hayo yote, BWANA aligeuza uteka wa
Ayubu.
“Basi huyo BWANA akaubarikia mwisho wa Ayubu
zaidi ya mwanzo wake, naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia efu
sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume
saba, binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili
akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika
nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wa Ayubu; na baba
yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu
akaishi miaka mia na arobaini, nae akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata
vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.” Ayubu 42:12-16
Ayubu alikataa Kukiri udhaifu, Kukiri misiba, Kukiri mateso
japo alikua kwenye mateso. Alisema, nalitoka tumboni kwa mama yangu ni uchi
nitarudi nikiwa uchi. Maandiko matakatifu yanasema; “Maana mwenye kuangalia upepo
hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna. Kama vile wewe usipojua njia ya
upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadharika
huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.” Muhubiri 11:4-5
Kwa imani
katika Kristo Yesu yatupasa kukataa yaliyokinyume na imani na tukiri yakuwa
anaweza kufanya mambo yote; Aweza
Kufungua Milango na Malango yaliyofungwa. Bwana Yesu Kristo anamtumia mtu aliye
tayari kutumika na si vinginevyo. Acha kujiua kwa maneno ya kinywa chako. Maana
yeye Kristo Yesu ni mwaminifu. Vaa na ujifunge SILAHA yako itakusaidia. “Basi
atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au
tuyawazayo kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.” Waebrania 3:20