SILAHA
NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;
SILAHA
YA SITA
GEUZA
UTEKA WAKO
Maombi yetu ni ya kufungua Malango na
Milango, sasa tunaingia hatua ya sita ya Kuvaa Silaha; Silaha ni lazima Ugeuze
kwa Maombi; uteka, taabu zako, Dhiki zako kuwa Baraka. Hali uliyopitia au
unayopitia haiwezi kugeuzwa kama wewe hutaigeuza
kwa Imani. Hakuna neno gumu la kumshinda kristo Yesu. Angalia mfano wa Ayubu; “Basi
ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo
Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako
wawili, kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama
alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na
kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya
kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa
nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu kwani ninyi hamkunena
maneno yaliyonyoka katka habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
Basi Elifazi, Mtemani na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda
wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru, naye BWANA akamridhia Ayubu. Kasha
BWANA akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye
akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea
nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala
chakula pamoja naye katika nyumba yake, nao wakamlilia na kumtuza moyo katika
habari za huo uovu wote BWANA aliouleta juu yake; kila mtu akam,pa kipande cha
fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho
wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na
ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na
wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima, na
wa pili akamwita jina lake Kesia, na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu.
Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa
Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kasha baada ya
mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana
wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawana
siku.” Ayubu 42:7-17
Pia tunajifunza kwa Yabesi katika Biblia
jinsi alivyofanya maombi ya kufungua milango na malango. Alipaza sauti yake kwa
Mungu wa Israeli ni kielelezo cha wenye haki, ni kweli kwamba Mungu huwabariki
wale ambao humuita kwa uaminifu. Yatupasa tuzingatie kwamba heshima na baraka
zitatujia na kutupata pale tutakapomwomba Mungu ndani mwa maombi ya kufungua
milango na malango. Yabesi anaonyesha waziwazi kwamba Baraka za Mungu na Ulinzi
wake havishuki kwetu hivihivi bali hutokea baada ya sisi kujitoa kwake na kwa
mpango wake hapa duniani na baadaya maombi yetu. Maombi ya Yabesi yaligeuza
historia ya maisha yake tena ya kuzaliwa nayo badala ya kuwa na maisha ya
huzuni alikuwa na maisha ya furaha. Maandiko yanathibitisha kielelezo cha
maisha ya Yabesi kama ifuatavyo; “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko
nduguze; na mamamye akamwita jina lake Yabesi, akisema, ni kwa sababu nalimzaa
kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba
ungenibarikia kwelikweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa
pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu
akamjalia hayo alioyaomba” 1Nyak 4:9-11
YABESI kwa lugha ya
kiebrania inasikia kama uchungu.
Tukimwomba Mungu kwa moyo wa dhati
pasipo shaka yeye ni mwaminifu kwa wote wamtafutao na kwake hakuna jambo lililo
gumu la kumshinda.“Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili, je! Kuna neno gumu
lolote nisiloliweza?” Yeremia
32:27
Malango na Milango, Inafunguliwa kwa
sisi Kuomba kwa kugeuza kimaombi kilicho kufa kipate kuwa hai. Ndani mwa maombi haya BWANA anasema waziwazi; “Watakuja
kwa kulia na kwa maombi nitawaongoza, nitawaendesha penye mito ya maji, katika
njia iliyonyooka, katika njia hiyo hawatajikwaa maana mimi ni baba wa Israeli…”
Yeremia 31:9
Maombi yanageuza hali, Maombi yanafungua
Malango yaliyofungwa. Bwana anasema Maana
nitageuza masikitiko yao kuwa furaha; nami nitawafanya waache huzuni zao.
Nasi tukiomba kwa Imani, Kristo Yesu atageuza uteka wetu kuwa Baraka. BWANA
aligeuza taabu ya Ayubu kuwa Baraka pia aligeuza msiba wa Ayubu kuwa baba wa
watoto wengi. Kwa kuwa Ayubu hakuteteleka katika imani bali aliomba na kukiri
akisema, “Lakini mimi najua ya kuwa mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye
atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini
pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na
macho yangu yatamtazama wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu!”
Ayubu 19:25-27
Wako maadui zako wanakutaja kwa ubaya;
wanasema mabaya juu yako, juu ya ndoa yako, wanasema mabaya juu ya kizazi
chako;
Lakini
Mungu atageuza tutakapodumu katika maombi ile laana na hayo matamko yao
yatakuwa Baraka.
“Kwa
sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri
Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa Baraka.”
Nehemia 13:2
Malango yalipofungwa mbele ya wana wa
Israeli, mtumishi wa Mungu Nehemia aliitisha maombi ya kufungua Malango na
milango muda wa miezi minne mfululizo. “Hata ikawa niliposikia maneno hayo,
nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba
mbele za Mungu wa mbinguni.” Nehemia 1:4
Hapa tunajifunza jinsi watakatifu wa
zamani walivyomwishia Mungu kwa imani. Kwa njia ya maombi na kujinyenyekeza kwa
kufunga, hatuoni mahali popote kimaandiko wakijihangaisha kutafuta mbinu
mbadala za kuwafungulia malango na milango katika maisha yao. Bali tunaona
silaha ya maombi ndiyo iliyotumika, tofauti na wakristo wa leo walio wengi
wameacha maombi, wameacha kufunga na kutafuta uso wa Mungu aliye hai,
wamegeukia imani nyingine za kutegemea vitu viitwavyo vya upako kama vile
mafuta ya upako, maji ya upako, chumvi ya upako, udongo wa upako, picha za hao
wajiitao manabii na mitume, vitambaa vya upako, sabuni za upako na vingine
vingi vifananavyo na hivyo. Vitu hivi haviwezi kamwe kuleta suluhisho la kiroho
katika maisha ya mkristo maana ni vitu vilivyobuniwa kwa akili za wanadamu sio
kwa akili za Mungu. Mkristo jifunze na ujiepushe na hizi imani potofu
zinazoenea kwa kasi zikionyesha zitafungua malango na milango ya watu wa Mungu
kumbe sivyo. Msingi wetu wa wokovu upo katika maneno haya; “Basi, kwakuwa sisi tu wazao wa
Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe,
vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili
za wanadamu.” Mdo 17: 29
Pia Mungu ni Roho na wale wanaomwabudu
Yeye sharti kumwabudu katika roho na kweli sio kwa mitazamo ya watu wanaopinga
maombi na kuwauzia watu vitu vya kiibada za kishetani ili viwalinde. “Basi
wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu msijemkachukuliwa na kosa
la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini kaeni katika
neema, na katika kumjua Bwana wetu na mwokozi Yesu Kristo, utukufu unayeye sasa
na hata milele.” 2Petro 3:17-18
Maana wengi walipotea kwa kufuata
uhalifu wa mioyo, maana kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama
vile kwetu watakavyo kuwepo waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi
wa kupoteza. Na wengi watafuata ufisadi wao, na wao watajipatia faida ya mali
kwa tamaa zao wenyewe wakitumia maneno yaliyotungwa ili kuwanasa yamkini
wateule. BWANA anasema, “Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu
yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliowekewa.”
2Petro 2:17
Wapenzi msiamini kila roho bali
zijaribuni hizo roho kwamba zimetoka kwa Mungu kwa sababu manabii wengi wa
uongo wametokea. Wenye kudanganya wanamfano wa utaua lakini wanazikana nguvu za
Mungu. Mkristo usidanganyike hakuna Mungu wa kweli anayepatikana ndani ya chupa
bali ndani mwa Maombi. Kristo Yesu alisema waziwazi; “Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni
nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” Mathayo 7:7
Ndugu zangu tangu zamani mafuta
yalikuwepo lakini hayakutumiwa kiholelaholela kama yanavyotumika sasa, ingekuwa
ni hivyo, Yesu Kristo asingewaagiza wanafunzi wake wasiondoke Yerusalemu mpaka
wajazwe nguvu za Roho mtakatifu. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia
juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na
katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Mdo 1:8 Kama mafuta yanaleta upaku au uwepo wa Mungu
angeweza kuwapaka mafuta akawaacha waende kutumika, lakini Kristo hakufanya
hivyo bali aliwaambia wakae mpaka siku ya Pentekoste (siku ya hamsini baada ya
kufufuka kwa Yesu) wakae kwenye maombi. “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste
walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa
upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliokuwa wameketi.
Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto ulio wakalia kila mmoja
wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama
Roho alivyowajaalia kutamka.” Mdo 2:1-4
Hivyo tukimwamini Mungu na nguvu zake,
yeye anazo nguvu na uweza mkuu wa kugeuza uteka wetu kuwa Baraka. Kila hali
unayoipitia iliyo ngumu hata kama ina historia tata kwa Mungu yote yawezekana
kwake yeye aaminiye. Simama katika zamu yako geuza uteka. Maandiko yanasema; “Uligeuza
matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.” Zaburi 30:11
Nyumba yako ifunike ndani mwa maombi ili
isiwe ni nyumba ya misiba, huzuni, umaskini, magonjwa, dhiki na vilio vya
uchungu. Bali zigeuza hali zote zisikaribie mlango wako. Usiogope, bali wewe
fanya Maombi upate kugeuza, Maana Mkono wake Kristo ni Mkono wenye Nguvu na
Uwezo mkuu wa kufungua malango na milango iliyofungwa. Tunajifunza kwa Mfalme
Yehoshafati aliwashinda wana wa Moabu na wana wa Amoni kwa Maombi ya kugeuza
ubaya wao uwapate wao wenyewe. “Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa
Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani.
Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, wanakuja jamii kubwa juu yako
watokao Shamu toka ng’ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari
(ndio En-gedi) Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA;
akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.” 2Nyakati 20:1-3
Wana wa Israeli walipokuwa ndani mwa
maombi ya kugeuza uteka; BWANA alilibatilisha shauri la maadui zao. Hata sisi
tukiomba kwa uaminifu na kwa juhudi, hakika maadui zetu wa kiroho na kimwili
wataanguka mbele yetu. Maana Mungu ni yeye yule jana, leo na hata milele.
“Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA
akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja
juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea
wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha
kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda
walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao angalia,
walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka.” 2Nyakati 20:22-24
Katika hili tunajifunza nguvu iliyomo
ndani mwa maombi maana tunauona mkono wa BWANA ambavyo unawaangusha maadui wa
Israeli walipokuwa kwenye maombi. Tuonapo vita katika ulimwengu wa roho au
mwili, hatua ya kwanza ni kumtafuta Mungu aliye hai kwa njia ya maombi. Ndipo
maadui zako wataanguka kwa ajili yako. Watu wa Moabu, Amoni na Seiri walipatana
kinyume juu ya Israeli lakini BWANA aligeuza shauri lao, panga zao na mikuki
yao, ikawachoma wenyewe ili yathibitike maneno ya Mungu yaliyonenwa na kinywa
cha nabii Isaya; “Utathibitika katika haki, utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana
hutaogopa, na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia. Tazama, yamkini
watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu
yako wataanguka kwa ajili yako. Tazama nimemuumba mhunzi avukutaye moto wa
makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemuumba mharibu ili aharibu. Kila
silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako
katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na
haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.” Isaya 54:14-17
Usiogope kwa sababu ya hayo bali yageuze
yawageukie wao wenyewe, maana wamechimba shimo lazima watumbukie wao. Geuza kwa
Maombi yako na kwa Dhabihu zako. Maana BWANA amekukumbuka tena na atakubarikia
tena. BWANA anasema; “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe,
usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia,
naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote
walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe
watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe;
watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu
yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume,
nikikuambia, usiogope; mimi nitakusaidia.” Isaya 41:10-13
Hakika tukiomba na tukaa ndani mwa
maombi; Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe;
watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu
yako.
0 comments:
Post a Comment