SILAHA
NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;
SILAHA YA SABA
UTOAJI WA DHABIHU
Kutoa
Dhabihu au Sadaka sio kununua kitu kwa Mungu bali ni ishara ya unyenyekevu
mbele za Mungu na ni tendo kamili la Kiibada. Kristo Yesu amefanyika Dhabihu ya
dhambi ili sisi tupate ukombozi. Mungu amemtoa Sadaka ili kupitia yeye
tufunguliwe mlango na milango ya mbinguni.
Utoaji wa dhabihu au sadaka ni wa muhimu sana kwake
yeye aaminiye maana tangu mwanzo dhabihu zilitolewa. Tunaona hata Adamu na Hawa
walipotenda dhambi, BWANA Mungu aliwafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi
akawavika. Lakini baada ya Mungu kumwinulia Adamu uzao walizaliwa Kaini na
Habili. kutokana na kazi zao walipewa nafasi sawa ya kumtumikia Mungu kwa kazi
za mikono yao. Kaini alikuwa mkulima na Habili alikuwa mfugaji. Tunajifunnza
kwa watu hawa wawili walikwenda kumtolea Bwana Mungu dhabihu (sadaka ya hiari) mbele za BWANA.
Maandiko yanathibitisha; “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya
ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na
sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabari Habili na sadaka yake; bali
Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akagadhibika sana, uso wake
ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, kwanini unaghadhabu? Na kwanini uso wako
umekunjamana?. KAMA UKITENDA VEMA, HUTAPATA KIBALI? Usipotenda vema dhambi iko
inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwanzo
4:3-6
Mungu
alimuumba mwanadamu kwa ajili yake. Ili amwabudu yeye, awe furaha yake iko
nafasi moja tu katika moyo wa mwanadamu ya ibada. Na hii ni kwa ajili ya Mungu
pekee. Mungu ni mwenye wivu asiyetaka kamwe kuchanganywa na miungu mingine.
Ndiyo maana Mungu aliweka amri katika amri kumi “Mimi ni Bwana Mungu wako
niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa usiwe na miungu
mingine ila mimi.” Kutoka 20:1-2
Suala
la kumwabudu Mungu linaambatana na kumtolea Mungu sadaka. Sadaka za wana wa
Adamu, Kaini na Habili inaonyesha kielelezo cha kumkaribia Mungu kwa ibada.
Tendo la kukubaliwa sadaka ya Habili ni kielelezo cha kukubaliwa mtoa sadaka.
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Kaini akamgadhibikia ndugu yake kwa sababu Mungu
alizikataa sadaka za Kaini kwa sababu moyo wake haukuwa mkamilifu. Maana BWANA
anasema, “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA bali maombi ya mtu mnyoofu ni
furaha. Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA. Bali humpenda mtu afuatie
wema.” Mithali 15:8-9
Ndiyo
maana hoja ya Mungu kwa Kaini inasema; KAMA UKITENDA VEMA, HUTAPATA KIBALI?
(If you do what is right, will you not be accepted?) Ili mtu wa Mungu dhabihu
yake ikubalike mbele za Mungu sharti awe na moyo mnyoofu. Habili anatajwa na
maandiko matakatifu ya kuwa ni shujaa wa imani aliyetoa sadaka iliyo bora
ambayo inanena mbele za Mungu. “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu
iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu
akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo ijapo amekufa angali akinena.” Waebrania
11:4
Mungu
aliikubali dhabihu ya Habili kwa sababu alikuwa mwenye haki na mtiifu. Nuhu
alipokwisha kuokolewa na Mungu yeye na jamaa yake toka kwenye gharika tunaona
anamjengea BWANA madhabahu na kutoa dhabihu. “Nuhu akamjengea BWANA madhabahu;
akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi,
akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya
kumridhisha; BWANA akasema moyoni, sitalaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu
ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala
sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.” Mwanzo
8:20-21
Baada
ya kuokolewa lazima tumkaribie Mungu kwa maombi na sadaka. Tunajifunza katika
utumishi wa Nuhu wa utoaji sadaka uliosababisha BWANA atoe tamko la kutokuangamiza
tena baada ya kusikia harufu nzuri ya sadaka nzuri zilizotolewa na Nuhu. Kwa
sadaka waweza kuikoa familia yako na maangamizi ufanyavyo hivyo ndani mwa
maombi. Mungu hakutoa tamko la kutokuangamiza tena kabla ya sadaka bali ni
baada ya sadaka kutolewa. Hivyo Mungu akambarikia Nuhu na wanae. Na akafanya
agano nao la kutofuta kizazi chao tena kwa gharika. “Na agano langu nitalithibitisha
nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya ghalika; wala
hakutakuwa tena ghalika, baada ya hayo kuiharibu nchi.” Mwanzo 9:11
Tunajifunza
pia kwa Ibrahimu baba yetu wa imani alimwabudu Mungu katika roho na kweli na
kutoa dhabihu juu ya madhababu. “BWANA akamtokea Abram, akasema, uzao wako
nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhababu BWANA aliyemtokea. Kisha
akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli,
akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa
mashariki, akamjengea BWANA madhababhu huko, kaliitia jina la BWANA.”
Mwanzo 12:7-8
Ibrahimu
aliitwa rafiki wa Mungu kwa sababu alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora, hata
alipokuwa amepewa mtoto Isaka, alipotakiwa kumtoa mwanawe mpendwa wa pekee
aliyempata katika uzee hakumzuilia Mungu. Tunasoma hivyo katika maandiko
matakatifu “… Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye Isaka, ukaende zako
mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko katika mlima mmoja wapo
nitakao kwambia… wakafika mahali pale walipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga
madhababu huko akaziweka tayari kuni kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka
juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa
kisu ili amchinje mwanawe… kwa maana sasa najua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo
hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee… kwa kuwa umetenda neno hili, wala
hukunizuilia mwano, mwanao wapekee, katika kukubariki nitakubariki, na katika
kukuzidisha nitakuzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga
ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao na katika uzao wako
mataifa yote duniani watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.” Mwanzo
22:1-18
Kwa
tendo hili Ibrahimu alihesabiwa kuwa mwenye haki pale alipomtoa mwanawe juu ya
madhabahu. Imani ya Ibrahimu ilijidhihirisha katika utii wa kweli kwa Mungu.
Yeyote atakaye kutembea na Mungu kwa karibu yampasa kuwa tayari kumtoa “Isaka” wake madhabahuni. Ibrahim
aliitwa rafiki wa Mungu kwa sababu ya kukubali kutoa Isaka wake. Wakristo wengi
wanatoa ili mradi wanatoa, hawatoi kilicho bora bali wanatoa bora sadaka.
Lakini tujifunze kwa watu hawa wawili Habili na Ibrahimu tunaona utoaji wao ni
utoaji ulio bora, walitoa sadaka zinazowagusa wao wenyewe, maana Isaka anatolewa mzima-mzima madhabahuni pa
BWANA. Hivyo hakuna kuabudu kuliko kamili kusiko ambatana na utoaji. Kila
mtu katika biblia aliyetoa sadaka bora ilidhihirisha ubora wa maisha ya mcha
Mungu. Maandiko yanathibitisha katika kitabu cha 1Nyakati “Mpeni BWANA utukufu wa jina
lake, leteni sadaka mje mbele zake; mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.”
1Nyakati 16:29
Kipindi
hiki cha nabii Eliya mtishibi alipotaka kukomesha imani potofu za miungu katika
Taifa la Israeli, zilizoanzishwa na mfalme Ahabu mwana wa Omri na mke wake
Yezebeli binti Ethbaali mfalme Wasidoni. Mfalme huyu na mke wake walimjengea
Baali madhabahu huko Samaria na wakamsujudia. Katika biblia mfalme Ahabu
anahesabika kuwa mfalme mwovu sana miongoni mwa wafalme wa Israeli. BWANA
alipokuwa amemwinua Eliya mtishibi kipindi hiki Ahabu alikuwa amewaua manabii
wengi mno wa Mungu aliye hai. Ilibidi afanye maombi ya kufunga malango na
milango juu ya Israeli, akaifunga mvua isinyeshe katika nchi miaka mitatu na
nusu (3½) maandiko yanasema; “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja
nasisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu yanchi muda
wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena mbingu zikatoa mvua, nayo nchi
ikazaa matunda.” Yakobo 5:17-18
Maombi
ya mwenye haki sharti yaambatane na kutoa dhabihu mbele za Mungu aliye hai,
tunajifunza kwa Eliya nabii.“Kisha Eliya akamwambia watu wote,
Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhahabu ya BWANA
iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana
wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, jina lako litakuwa
Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya
mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha
akazipanga zile kuni, akamkata-kata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu
ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya
kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema fanyeni mara ya pili, wakafanya mara ya
pili. Akasema fanyeni mara ya tatu, wakafanya mara ya tatu. Yale maji
yakaizunguka madhabahu, akaujaza mfereji maji. Ikawa wakati wa kutoa dhabihu ya
jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa
Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli,
na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno
lako. Unisikie, Ee BWANA unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA,
ndiwe Mungu, na ya kuwa wew umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA
ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, yaliyokuwamo
katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA
ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata
mmoja, wakawakamata, na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua
huko.” 1Wafalme 18:30-46
Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa
Yakobo, akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; tunajifunza
tendo la imani kwa mtumishi wa Mungu nabii Eliya jinsi alivyobeba watu wake kwa
kabila zao na kuwainua mbele za BWANA kwa njia ya maombi, kisha akazipanga zile kuni,
akamkata-kata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni.
Tunajifunza kuwa maombi na dhabihu vinakwenda pamoja madhabahuni pa BWANA. Ikawa
wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA,
Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe
ndiwe Mungu katika Israeli, Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza
sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu
wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu.
Moto
wa BWANA unawakilisha uwepo wa Mungu na nguvu zake. Maombi haya ya kufungua
Malango na Milango sharti yaambatane na Kutoa Dhabihu mbele za Mungu
aliye hai. Eliya Mtishibi ili akomeshe taabu, dhiki na mateso kwa Israeli
vilivyotekwa na mfalme Ahabu na mkewe Yezebeli kwa kuungamanisha taifa kwa
miungu ya Wasidoni mungu aitwaye Baari na Ashtoleth; Eliya alisimama mahali
palipo bomoka, akajenga Madhabahu ya BWANA tena iliyokuwa imevunjika. Kwa mawe
kumi na mawili sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli.
Hata Mungu mwenyewe, ili amwokoe mwanadamu na dhambi, alimtoa mwanawe wa pekee
Yesu kristo, ili awe kuhani mkuu atakaye wapatanisha kwa njia ya kifo cha
msalaba. Ili kwa damu yake Kristo Yesu wanadamu wapate ukombozi maana pasipo
damu hakuna ondoleo la dhambi. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee,
bali awe na uzima wa milele.” Yohana
3:16
Vitu
vyote tulivyo navyo vyatoka kwake na viko kwa uweza wake, hivyo tunapotoa
Dhabihu zetu mbele zake yeye Mungu aliye hai ni tendo la Kiimani la
Kujiungamanisha naye kwa neno na kwa tendo.
“Au
ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena? Kwa kuwa vitu vyote
vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye
milele. Amina.” Warumi
11:35-36
Maombi
yetu ya kufungua malango sharti yatubebe Sisi, Watoto wetu na Mali zetu. “Na
tumwinulie Mungu aliye mbinguni, Mioyo yetu na mikono.” Maombolezo 3:41
Maana
yake; Wewe binafsi ufunguliwe Malango na Milango, Watoto wako wafunguliwe
Malango na Milango, Mali zako, Kazi yako, Biashara yako, Elimu yako na Vyote
Uvitendavyo vistawishwe katika BWANA visizae Kufa-kufa wala Mapooza.
“Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote, Ndipo ghala
zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.” Mithali 3:9-10
Bwana
yeye ndiye atupaye Baraka na Ustawi si vinginevyo, Lazima tujinyenyekeze kwa
Maombi yeu na Sadaka zetu zilizo bora. “Ana wingi wa siku katika mkono wake wa
kuume, UTAJIRI na HESHIMA katika mkono wake wa kushoto. NJIA zake ni njia za
kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao
wamshikao sana, Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.” Mithali 3:16-18
Baraka
za Mungu zipo kwao waliotayari kuzifuata na kushikamana nazo. Unapo mwomba
Mungu na kutoa Dhabihu zako Madhabahuni pake, Yeye hushuka kwa nguvu zake na
atakupa Baraka zifuatazo:-
(i) WINGI WA SIKU; maana yake Maisha
marefu.
BWANA anasema; “Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano
ulivyo wakati wake.” Ayubu 5:26
(ii)
UTAJIRI
na HESHIMA;
Vinaambatana na USTAWI katika kazi yako
yote ya mikono. “Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu.
Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.” Mithali 8:20-21
Jambo
la msingi lazima kila mmoja wetu anayeitwa kwa jina la BWANA, sharti ajenge
Madhabahu ya BWANA kwa ajili yake na familia yake. Maana yake ni Kumrejesha
Mungu wa kweli katika familia. Panahitajika mtu atakaye batilisha hiyo miungu
ya ukoo, miungu ya kichifu, isitende kazi kwa kuivua madhabahuni kwa njia ya
maombi na dhabihu ili maandiko yatimie ya Mtunga Zaburi. “Hawa wanataja magari na hawa
farasi, Bali sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu. Wao wameinama na
kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.” Zaburi 20:7-8
Baada
ya kuokoka na kuvishwa uwezo wa ki-Mungu kwa njia ya imani yatupasa kuchukua
hatua za kiimani ndani mwa maombi ili KUBATILISHA
na KUTENGUA ibada za miungu na
matoleo yake (makafara), yaliyotolewa kabla. Ibada za miungu hufanyika kwa njia
ya maombi na dhabihu japo hazitolewi kwa mungu wa kweli lakini mfumo unaweza
kufanana na wa ibada za kweli, ndiyo maana manabii wa Baali walijenga madhabahu
na kutoa sadaka. Tunaona katika maandiko; “Eliya akawaambia manabii wa Baali,
jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeneza kwanza; maana ninyi ndio wengi;
mkaliitie jina la mungu wenu wal msitie moto chini… wakaliitia jina la Baali
tangu asubuhi hata adhuhuri wakisema Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na
sauti, wala aliye jibu. Nao wakrukaruka juu ya madhabahu aliyoifanya… ikawa
wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni;
lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.” 1Wafalme
18:25-29
Tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Ayubu
jinsi alivyoomba na kutoa dhabihu kwa Mungu aliye hai; Ayubu alikuwa anawaombea daima watoto wake na kuwatolea
dhabihu mbele za BWANA, kila mmoja alimtolea Maombi na Sadaka. Hata Shetani alipowatamani
watoto wa Ayubu na akatamani kumfilisi Ayubu, alishindwa mpaka alipomwendea
Mungu kuomba apewe ruhusa.
Maisha
ya Ayubu na familia yake yalijulikana daima mbele za BWANA. Tunasoma katika
maandiko matakatifu yanasema; “Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao
zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi
namapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa;
kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru
Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote. Ilikuwa, siku moja
ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye
akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu
BWANA, na kusema Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea
huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, je! Umemwangalia huyo
mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu
mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani
akamjibu BWANA, na kusema, je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira
kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi
za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake umeiongezeka katika nchi.” Ayubu
1:5-10
Ayubu
hakuwaacha watoto wake nyuma katika Ibada, bali aliwabeba daima na kuwaombea.
Mungu alimzingira pande zote yeye na familia yake pamoja na mali zake zote,
BWANA aliwawekea UKINGO, shetani akashindwa kuwanasa.
Tunapata
siri ya ki-Mungu ya kwamba tumwombapo Mungu na kutoa dhabihu zinazokubalika
mbele zake, Yeye hutuwekea ukingo pande zote. Ukingo maana yake ni ukuta, boma,
ngome, jabali, mwamba. Na BWANA anasema; “Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta
wa moto kuuzunguka pande zote nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.”
Zekaria 2:5
Lazima
uchukue hatua ya Kiimani kumwendea Mungu Madhabahuni pake. Omba, Ombea,
Watiishe watoto wako kwenye Maombi na Sadaka popote walipo na adui hatawanasa
kamwe. “Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na
vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake
umeiongeza katika nchi.” Ayubu
1:10
Inua
Biashara yako mbele za BWANA, Inua kazi yako mbele za BWANA, Inua Elimu yako
mbele za BWANA kwa maombi na sadaka. “Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Leteni
sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.” 1
Mambo ya nyakati 16:29
Leteni
Sadaka, mje mbele zake, Inua mikono mje mbele zake kwa Maombi ili BWANA aweke
Ukingo kwako, Mabaya yasikupate na Ulinzi wake ukufunike.
Tunaona
mtumishi wa Mungu mfalme Daudi alipokuwa na msiba uliotokana na pigo la ugonjwa
wa tauni toka kwa BWANA. Maelfu ya watu yamekwishakufa katika nchi yake, wakati
Daudi hajui cha kufanya ili kuondoa mauti juu ya nchi ndipo anaambiwa na Mungu
ajenge Madhabahu na atoe Dhabihu. “Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi,
akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha
Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama BWANA
alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia,
Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema,
Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema,
Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili kwamba
tauni ipate kuzuiliwa katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme
na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake, tazama ng’ombe hawa kwa sadaka
ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe, viko kwa kuni.
Vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna
akamwambia mfalme, BWANA Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia
Arauna, La, sivyo lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake, wala
sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizo zigharamia. Hivyo
Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekel hamsini
za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za
kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliidhiria nchi, na tauni ikazuiliwa
katika Israeli.” 2 Samweli
24:18-25
Tunajifunza
kwa mtumishi wa Mungu Daudi jinsi alivyotoa Sadaka yenye gharama na bora aliyo gharamikia
yeye mwenyewe. Matokeo yake tunayaona baada ya Daudi kutoa dhabihu kifo
kilizuiliwa kwa watu wake. Tukio hili ni la kiimani na la kuigwa kwa watu wa
Mungu. Tunayaona Maombi ya kufungua Malango na Milango ni sharti tumwendee
Mungu madhabahuni, Tumjengee madhabahu na Tutoe Sadaka; naye atashuka Kuzuia
Magonjwa, Mateso, Misiba na kila aina ya Vifungo. Hivyo Usiogope; Jenga
Madhabau yako, Toa Sadaka, hayo yaliyokupata yataondolewa na kuzuiliwa yasije
kwako tena. Dhabihu yako, Igeuze Msiba wako kuwa Uzima, na kwa wale unao
waombea na kuwainua mbele za Mungu aliye hai.
“Atoaye
dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.” Zaburi 50:23
Lazima
nasi tunapofunguliwa Malango na Milango; fahamu wako wengi watupingao watatufuata-fuata kwa ubaya, Nawe usimamapo katika maombi
nyosha mkono wako juu yao, kinyume, warudishie mabaya yao, yawalambe, wavishwe
fedheha yao. “Bwana akamwambia Musa, nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji
yarudi tena juu ya wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa
akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa
nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao
Wasmisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi,
hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata
mtu mmoja.” Kutoka 14:26-28
Usiudharau
Mkono wako, Musa aliponyoosha mkono wake juu ya bahari, BWANA alifungua njia na
mlango kwa wana wa Israel wakapita, Bahari ikawa nchi kavu. Nasi tukinyosha
mikono yetu kwa Jina la Yesu Kristo yatafanyika na Malango yatafunguka. “Maovu
yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.” Mithali 5:22
0 comments:
Post a Comment