Friday, 28 November 2014


Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu unayefuatilia kwa ukaribu makala haya. Nakusalimu katika jina la BWANA wetu Yesu Kristo.

Bado tunaendea na mfululizo wa makala haya ambayo yanakujia kila wiki na usisite kuuliza maswali endapo hutaelewa kipengele chochote katika mfululizo huu.


Wiki jana nilikufundisha juu ya aina za funguo za kufungua malango na milango, ambapo nilikwambia zipo aina tano na nikakufundisha funguo mbili kati ya hizo. Funguo ya kwanza ilikuwa ni Neno la Mungu na ya pili ilikuwa ni Imani.

Nilikwambia ya kuwa neno la Mungu ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza na Nguvu za ki-Mungu zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili. Pia nilikuonesha maandiko ambayo yanathibitisha hilo.

Katika kipengele cha imani ambacho ndicho tunachoendela nacho siku ya leo, nilikufundisha maana halisi ya imani na nilisema  Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile Mungu alichokisema katika Neno lake.

Nilizama zaidi  na kukuonesha msingi wa kuwa na imani kwa Mungu ambao uko katika kweli tatu zilizobebwa na maana halisi ya Asili ya Mungu wetu. Kweli hizo ni  Hawezi Kubadilika, Hawezi Kushindwa na Hawezi Kudanganywa.

Endelea……….

Malango na Milango ni sharti ifunguliwe kwa Imani; sawasawa na Neno la Mungu. Kwa Imani tunalegeza viuno vya wafalme, Kwa Imani tunalegeza mafungo na vifungo vilivyowafunga watu wa Mungu. Kwa Imani tunafungua Malango na Milango iliyofungwa mbele yetu.

 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Isaya 10:27

Kila mzigo uliotwishwa katika nafsi yako unaondolewa begani mwako maana uwezo wake Kristo Yesu sasa umedhihirishwa ili kazi zote za yule mwovu shetani zivunjwe ndani mwa imani.

“Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo, nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.” Zekaria 10:2

Imani ni Ufunguo wa kufungua Malango na  Milango, tunaona Senakeribu analeta majeshi yake akiwa ameazimia kupiga watu wa Mungu na kuwatawala. Mfalme Hezekia  akasema na watu wake ili apate wakuwajenga Kiimani.

 “Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye, kwake upo mkono wa mwili, ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia mfalme wa Ashuru.” 2Mambo ya Nyakati 32:7-8

Adui anakuja na neno lenye kuogofya ili kuifisha Imani yako, Senekarabu anatuma watu wenye kuhubiri hofu kwa kueleza historia ya Hezekia ya udhaifu.
Senekerebu anatuma watu wake wageuze neno la Mfalme Hezekia ili apate kuifisha Imani yao apate kuwapiga. Hezekia anataka kuonyesha waziwazi tofauti kati ya mkono wa mfalme wa Ashuru na mkono wa BWANA.

Nasi kanisa lazima tutambue ya kuwa kwetu upo mkono wa BWANA wenye nguvu ya Kuokoa na Kuponya hivyo lazima tusimame kwa Imani ndipo tupate kufungua Malango na Milango iliyofungwa mbele zetu, Maana pasipo IMANI haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa imani yote yanawezekana katika Kristo.

Imani ni chanzo kikuu cha kupokea kutoka kwa Mungu maana hakuna neno lolote lililo gumu la kumshinda Mungu aliye hai.

Mwanamke huyu aliteseka pamoja na kuteswa na mengi lakini kwa IMANI alipata kupokea Uponyaji baada ya kusikia Neno la Yesu Kristo lenye nguvu ya Kuponya. Hivyo kwa imani Wagonjwa wataponywa na kupata afya tena.

Wakati mwanamke yule anashika pindo la vazi la Yesu Kristo, nguvu zilizomtoka Yesu Kristo, ndizo zilizokwenda kufanya uponyaji kwa mwanamke huyu kwa Imani, hivyo ni dhahiri pasipo Imani hakuna nguvu ya Mungu kuingia na kuponya. Unaweza kuguswa na Watu au Watumishi wa Mungu na usipone lakini ukiamini kabisa na usione shaka moyoni mwako hapo ndipo utakapo pokea.“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kkwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”  Warumi 10:9-10

Imani yetu katika Yesu Kristo Yesu sharti ivuke mipaka iliyowekwa mbele yetu, maana kwa Imani BWANA anasema,
“Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza, nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma.” Isaya 45:2

WATU WANAWEZA KUKUCHEKA KWASABABU YA IMANI YAKO KATIKA MUNGU, usiogope vicheko vyao bali kaza roho kwa Imani maana lipo Jibu kwa kuwa Mungu hufungua njia mahali pasipo kuwa na njia. Angalia mfano huu wa ufunguo wa imani; “

 “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, aliposikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, wakamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwambo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi, tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile, akaamuru apewe chakula.” Marko 5:35-43

Katika msiba Yesu anaangalia imani ya yule mkuu wa Sinagogi ili apate kutenda muujiza. Kwa maana Imani ahitaji ushabiki wa watu bali Imani inahitaji mtu mwenye kujua Neno la Mungu na kuliamini. Watu walimcheka Yesu Kristo pale aliposema mtoto hajafa bali amelala, Yesu akamwamsha, akamwambia kijana amka naye akawa mzima. Vivyo hivyo inawezekana upo kwenye ndoa miaka mingi hujapata mtoto, Kwa Imani tumbo lako lifunguliwe milango yake na upate watoto wa kiume na wakike.

 “Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba, alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.” Waebrania 11:11

SARA alipoambiwa atabeba mimba na kuzaa aliona ni kichekesho kwake maana alikuwa mzee. Hali halisi ya mwili wa Sara ilimfanya apoteze imani ya kuzaa. Wako watu wengi wa Mungu wanaopishana na Baraka zao toka kwa BWANA kwa sababu ya kuhesabu miaka ya mapito yao na kuona Mungu amechelewa na kinachozaliwa ni kukata tamaa kwa mfano wa Sara. “Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.” Mwanzo 18:11-14

Katika mambo yote Mungu hufanya kazi na wenye Imani ili apate kuwapatia Mema kwani ndio wale walioitwa kwa kusudi lake, Sisi tu watoto wa Mungu basi sasa tu warithi wa Baraka na Ustawi wa Kimungu, turithio kwa Imani pamoja na Kristo Yesu. Imani ni kutarajia yasiyowezekana kutarajiwa.

SARA alimpokea Isaka katika hali ya kutokutarajiwa kwani alikuwa mkongwe wa miaka mingi. Tangu Mungu atamke Ahadi ya uzao wa Sara, miaka ishirini na tano ilipita. “Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abrahamu akenda kama BWANA alivyomwamuru, Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.” Mwanzo 12:3-4

IBRAHIMU alishakata tama juu ya ahadi ya Mungu ya kupata mtoto kupitia SARA, maana kimwili Sara alikuwa ni mzee asingeweza tena kuzaa. (biologically)
“Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme za kabila za watu watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.”  Mwanzo 17:15-18

 Kwa imani kila mlango uliofungwa utafunguliwa, hatuhitaji kuangalia historia uliyopitia au hali ya mwili wako bali unachopaswa kuangalia ni Uweza na Nguvu za Mungu aliyehai ambaye yeye hashindwi na jambo lolote.

 “…lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.” Habakuki 2:4

“BWANA ametukumbuka, naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni, Atawabariki wamchao BWANA, wadogo kwa wakubwa.” Zaburi 115:12-13

Ushindi wetu katika ulimwengu wa Roho na mwili hutegemea Ufunguo wa Imani.

Itaendelea……..



0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget