Friday 21 November 2014

Mch. Florian . J. Katunzi.
Bwana asifiwe mtu wa Mungu, bado naendelea na mtiririko wa somo hili ambaloninaamini litafanyika msaada kwako na hata kwajirani yako. Pia napenda kukumbusha ya kuwa kitabu hiki kitatoka  siku chache zijazo hivyo jiandae kukipokea.

Katika utangulizi wa somo hili tuliangalia juu ya habari za Mfalme Nebukadreza aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo na pia alikuwa muabudu miungu. Mara  baada ya kifo chake Mungu alimuinua Mfalme Koreshi ambaye alikuwa mpakwa mafut wa BWANA na alifanya akusudi yote ambayo Mungu aliyaweka.

 Leo tutakwenda kuangalia juu ya aina tano za funguo za kufungua                                               malango na   milango. 


 AINA TANO ZA FUNGUO ZA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO;


 UFUNGUO WA KWANZA 

 NENO LA MUNGU   


 Neno ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza na Nguvu za ki-Mungu zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili. Yesu Kristo alithibitisha yakuwa Neno la Mungu lina mamlaka na nguvu pale alipolitumia kufungua mafungo yaliyofunga watu wa Mungu sawasawa na injili ya Luka 4:36 Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, ni Neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.” 


Tunajifunza pia kwa Neno vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viliumbwa maana Mungu aliziumba mbingu na nchi kwa Neno lake. Alisema iwe na ikawa. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yohana 1:1-5


 Tukitaka kufungua malango na milango iliyofungwambele yetu sharti kwanza tuwe na ufunguo wa Neno la Mungu. Maana Neno ni taa na nuru ya maisha yetu. Aliye na Neno haendi gizani kwa sababu kwa Neno la Mungu hakuna lisilowezekana.Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Luka 1:37


 Neno la Mungu kamwe halipiti hivyo tukilishika Neno kila lango na malango hakika yatafunguka. “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe” Mathayo 24:35Neno lake husimama katika kweli daima. Neno la Mungu huja kwetu likiwa hai, likifungulia imani yetu.Ndipo BWANA akaniambia… naliangalia neno langu, ili nilitimize” Yeremia 1:12
 

 UFUNGUO WA PILI

IMANI


Imani sikuzote imekuwa ndiyo alama ya wanafunzi wa Yesu. Wanafunzi wa kwanza walijulikana kama WAAMINI. Yesu alisema “… Yote yawezekana kwake aaminiye Mark 9:23


Imani humaanisha kumtegemea Mungu kwa hali zote. Wakati Adamu alipofanya dhambi, alijitoa katika kumtegemea Mungu na kujitegemea (ambako ni kutokuamini). Hii ndiyo sababu Mungu ameweka kipaumbele kwenye imani. Imani ni njia ya kuturudishia uhusiano na Mungu (kumtegemea Mungu). Basi Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Warumi 10:17  


Tunajifunza yakuwa pasipo Neno la Mungu hakuna imani ya ki-Mungu. Maana yake ufunguo wa kwanza ndiyo unaotupeleka kwenye ufunguo wa pili. Kumtegemea Mungu ndiko kunakoitwa imani. Kwa imani unatoka kwenye kutokuweza hadi kuweza. Kwa imani hakuna lisilowezekana.


 A: IMANI NI NINI?  


Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile Mungu alichokisema katika Neno lake.Imani ya kweli inaelezewa katika Utii na Kutenda kulingana na  Neno la Mungu.Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” Waebrania 11:1


Hivyo pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu; kwa maana kila mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, naye huwapa thawabu wale wamtafutao sawasawa na Neno lake. Ni lazima tumtafute Mungu kwa juhudi na kutamani kwa bidii uwepo wa neema yake.


Imani na utii haviwezi kutengana kama vile ambavyo kutokuamini na kutokutii kusivyoweza kutengana.Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; hawakuigopa amri ya mfalme. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabiwa ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa  imani akatoka Misri asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”  Waebrania 11:23-27 


B: KWELI TATU ZA IMANI    


 Msingi wa kuwa na imani kwa Mungu uko katika kweli tatu muhimu: Asili ya Mungu; 

 a.     Hawezi Kubadilika.
“Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu..” Malaki 3:6
 b.     Hawezi Kushindwa“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na yakuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika” Ayubu 42:2
 c.      Hawezi Kudanganywa“Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” Hesabu 23:19
Kristo amefanyika chanzo cha imani yetu kwa Mungu. Ukweli kuhusu kifo chake na ufufuko hutoa msingi wa kuamini kwetu.Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi” 1Wakorintho 1:30


Ili imani itende kazi ya kufungua malango na milango katika maisha yetu, ni lazima kutii Neno la Mungu. Imani HUTENDA KAZI pale mtu aliyeamini anapofanya sehemu yake kwa imani, hiyo humfanya Mungu naye kutenda sawasawa na kuamini kwa mtu. 


Angalia mfano wa mwanamke aliyekuwa na msiba wa kutokwa damu muda wa miaka kumi na miwili, aliposikia Neno la uponyaji kupitia Kristo Yesu aliamini na kuadhimia moyoni mwake kumwendea Yesu Kristo kwa imani ili apate kufunguliwa. “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi namiwili alikuja kwa nyuma, akagusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Mathayo 9:20-21


Matokeo ya imani sikuzote mwisho wake ni ushindi kwake yeye aaminiye na kumletea utukufu wa Mungu katika maisha yake ya kiroho na kimwili. “… kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu” 1Yohana 5:4


Malango na Milango ni sharti ifunguliwe kwa Imani; sawasawa na Neno la Mungu. Kwa Imani tunalegeza viuno vya wafalme, Kwa Imani tunalegeza mafungo na vifungo vilivyowafunga watu wa Mungu. Kwa Imani tunafungua Malango na Milango iliyofungwa mbele yetu.  “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Isaya 10:27


 Kila mzigo uliotwishwa katika nafsi yako unaondolewa begani mwako maana uwezo wake Kristo Yesu sasa umedhihirishwa ili kazi zote za yule mwovu shetani zivunjwe ndani mwa imani. “Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo, nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.” Zekaria 10:2


Imani ni Ufunguo wa kufungua Malango na  Milango, tunaona Senakeribu analeta majeshi yake akiwa ameazimia kupiga watu wa Mungu na kuwatawala. Mfalme Hezekia  akasema na watu wake ili apate wakuwajenga Kiimani.  “Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye, kwake upo mkono wa mwili, ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia mfalme wa Ashuru.”   2 Mambo ya Nyakati 32:7-8


 Adui anakuja na neno lenye kuogofya ili kuifisha Imani yako, Senekarabu anatuma watu wenye kuhubiri hofu kwa kueleza historia ya Hezekia ya udhaifu.Senekerebu anatuma watu wake wageuze neno la Mfalme Hezekia ili apate kuifisha Imani yao apate kuwapiga. Hezekia anataka kuonyesha waziwazi tofauti kati ya mkono wa mfalme wa Ashuru na mkono wa BWANA. 


Nasi kanisa lazima tutambue ya kuwa kwetu upo mkono wa BWANA wenye nguvu ya Kuokoa na Kuponya hivyo lazima tusimame kwa Imani ndipo tupate kufungua Malango na Milango iliyofungwa mbele zetu, Maana pasipo IMANI haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa imani yote yanawezekana katika Kristo.


 Imani ni chanzo kikuu cha kupokea kutoka kwa Mungu maana hakuna neno lolote lililo gumu la kumshinda Mungu aliye hai. Mwanamke huyu aliteseka pamoja na kuteswa na mengi lakini kwa IMANI alipata kupokea Uponyaji baada ya kusikia Neno la Yesu Kristo lenye nguvu ya Kuponya. Hivyo kwa imani Wagonjwa wataponywa na kupata afya tena.


Wakati mwanamke yule anashika pindo la vazi la Yesu Kristo, nguvu zilizomtoka Yesu Kristo, ndizo zilizokwenda kufanya uponyaji kwa mwanamke huyu kwa Imani, hivyo ni dhahiri pasipo Imani hakuna nguvu ya Mungu kuingia na kuponya. Unaweza kuguswa na Watu au Watumishi wa Mungu na usipone lakini ukiamini kabisa na usione shaka moyoni mwako hapo ndipo utakapo pokea.Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kkwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”  Warumi 10:9-10


Imani yetu katika Yesu Kristo Yesu sharti ivuke mipaka iliyowekwa mbele yetu, maana kwa Imani BWANA anasema,Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza, nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma.” Isaya 45:2


 WATU WANAWEZA KUKUCHEKA KWASABABU YA IMANI YAKO KATIKA MUNGU, usiogope vicheko vyao bali kaza roho kwa Imani maana lipo Jibu kwa kuwa Mungu hufungua njia mahali pasipo kuwa na njia. Angalia mfano huu wa ufunguo wa imani; “  “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, aliposikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, wakamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwambo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi, tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile, akaamuru apewe chakula.” Marko 5:35-43


 Katika msiba Yesu anaangalia imani ya yule mkuu wa Sinagogi ili apate kutenda muujiza. Kwa maana Imani ahitaji ushabiki wa watu bali Imani inahitaji mtu mwenye kujua Neno la Mungu na kuliamini. Watu walimcheka Yesu Kristo pale aliposema mtoto hajafa bali amelala, Yesu akamwamsha, akamwambia kijana amka naye akawa mzima. Vivyo hivyo inawezekana upo kwenye ndoa miaka mingi hujapata mtoto, Kwa Imani tumbo lako lifunguliwe milango yake na upate watoto wa kiume na wakike.  “Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba, alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.” Waebrania 11:11


SARA alipoambiwa atabeba mimba na kuzaa aliona ni kichekesho kwake maana alikuwa mzee. Hali halisi ya mwili wa Sara ilimfanya apoteze imani ya kuzaa. Wako watu wengi wa Mungu wanaopishana na Baraka zao toka kwa BWANA kwa sababu ya kuhesabu miaka ya mapito yao na kuona Mungu amechelewa na kinachozaliwa ni kukata tamaa kwa mfano wa Sara. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.” Mwanzo 18:11-14


Katika mambo yote Mungu hufanya kazi na wenye Imani ili apate kuwapatia Mema kwani ndio wale walioitwa kwa kusudi lake, Sisi tu watoto wa Mungu basi sasa tu warithi wa Baraka na Ustawi wa Kimungu, turithio kwa Imani pamoja na Kristo Yesu. Imani ni kutarajia yasiyowezekana kutarajiwa. SARA alimpokea Isaka katika hali ya kutokutarajiwa kwani alikuwa mkongwe wa miaka mingi. Tangu Mungu atamke Ahadi ya uzao wa Sara, miaka ishirini na tano ilipita. Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abrahamu akenda kama BWANA alivyomwamuru, Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.” Mwanzo 12:3-4 


IBRAHIMU alishakata tama juu ya ahadi ya Mungu ya kupata mtoto kupitia SARA, maana kimwili Sara alikuwa ni mzee asingeweza tena kuzaa. (biologically)Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme za kabila za watu watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.”  Mwanzo 17:15-18


Kwa imani kila mlango uliofungwa utafunguliwa, hatuhitaji kuangalia historia uliyopitia au hali ya mwili wako bali unachopaswa kuangalia ni Uweza na Nguvu za Mungu aliye hai ambaye yeye hashindwi na jambo lolote.  “…lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.” Habakuki 2:4


BWANA ametukumbuka, naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni, Atawabariki wamchao BWANA, wadogo kwa wakubwa.” Zaburi 115:12-13


 Ushindi wetu katika ulimwengu wa Roho na mwili hutegemea Ufunguo wa Imani.

Itaendelea……………………..

0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget