Thursday 28 May 2015

SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;

SILAHA YA SITA

GEUZA UTEKA WAKO
Maombi yetu ni ya kufungua Malango na Milango, sasa tunaingia hatua ya sita ya Kuvaa Silaha; Silaha ni lazima Ugeuze kwa Maombi; uteka, taabu zako, Dhiki zako kuwa Baraka. Hali uliyopitia au unayopitia haiwezi kugeuzwa kama  wewe hutaigeuza kwa Imani. Hakuna neno gumu la kumshinda kristo Yesu. Angalia mfano wa Ayubu; “Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili, kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katka habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi Elifazi, Mtemani na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru, naye BWANA akamridhia Ayubu. Kasha BWANA akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake, nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote BWANA aliouleta juu yake; kila mtu akam,pa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima, na wa pili akamwita jina lake Kesia, na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kasha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawana siku.” Ayubu 42:7-17

Pia tunajifunza kwa Yabesi katika Biblia jinsi alivyofanya maombi ya kufungua milango na malango. Alipaza sauti yake kwa Mungu wa Israeli ni kielelezo cha wenye haki, ni kweli kwamba Mungu huwabariki wale ambao humuita kwa uaminifu. Yatupasa tuzingatie kwamba heshima na baraka zitatujia na kutupata pale tutakapomwomba Mungu ndani mwa maombi ya kufungua milango na malango. Yabesi anaonyesha waziwazi kwamba Baraka za Mungu na Ulinzi wake havishuki kwetu hivihivi bali hutokea baada ya sisi kujitoa kwake na kwa mpango wake hapa duniani na baadaya maombi yetu. Maombi ya Yabesi yaligeuza historia ya maisha yake tena ya kuzaliwa nayo badala ya kuwa na maisha ya huzuni alikuwa na maisha ya furaha. Maandiko yanathibitisha kielelezo cha maisha ya Yabesi kama ifuatavyo; “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamamye akamwita jina lake Yabesi, akisema, ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kwelikweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo alioyaomba” 1Nyak 4:9-11

YABESI kwa lugha ya kiebrania inasikia kama uchungu.
Tukimwomba Mungu kwa moyo wa dhati pasipo shaka yeye ni mwaminifu kwa wote wamtafutao na kwake hakuna jambo lililo gumu la kumshinda.“Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili, je! Kuna neno gumu lolote nisiloliweza?”  Yeremia  32:27

Malango na Milango, Inafunguliwa kwa sisi Kuomba kwa kugeuza kimaombi kilicho kufa kipate kuwa hai. Ndani mwa maombi haya BWANA anasema waziwazi; “Watakuja kwa kulia na kwa maombi nitawaongoza, nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka, katika njia hiyo hawatajikwaa maana mimi ni baba wa Israeli…” Yeremia 31:9

Maombi yanageuza hali, Maombi yanafungua Malango yaliyofungwa. Bwana anasema Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha; nami nitawafanya waache huzuni zao. Nasi tukiomba kwa Imani, Kristo Yesu atageuza uteka wetu kuwa Baraka. BWANA aligeuza taabu ya Ayubu kuwa Baraka pia aligeuza msiba wa Ayubu kuwa baba wa watoto wengi. Kwa kuwa Ayubu hakuteteleka katika imani bali aliomba na kukiri akisema, “Lakini mimi najua ya kuwa mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na macho yangu yatamtazama wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu!” Ayubu 19:25-27  


Wako maadui zako wanakutaja kwa ubaya; wanasema mabaya juu yako, juu ya ndoa yako, wanasema mabaya juu ya kizazi chako;
Lakini Mungu atageuza tutakapodumu katika maombi ile laana na hayo matamko yao yatakuwa Baraka. “Kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa Baraka.” Nehemia 13:2

Malango yalipofungwa mbele ya wana wa Israeli, mtumishi wa Mungu Nehemia aliitisha maombi ya kufungua Malango na milango muda wa miezi minne mfululizo. “Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni.” Nehemia 1:4

Hapa tunajifunza jinsi watakatifu wa zamani walivyomwishia Mungu kwa imani. Kwa njia ya maombi na kujinyenyekeza kwa kufunga, hatuoni mahali popote kimaandiko wakijihangaisha kutafuta mbinu mbadala za kuwafungulia malango na milango katika maisha yao. Bali tunaona silaha ya maombi ndiyo iliyotumika, tofauti na wakristo wa leo walio wengi wameacha maombi, wameacha kufunga na kutafuta uso wa Mungu aliye hai, wamegeukia imani nyingine za kutegemea vitu viitwavyo vya upako kama vile mafuta ya upako, maji ya upako, chumvi ya upako, udongo wa upako, picha za hao wajiitao manabii na mitume, vitambaa vya upako, sabuni za upako na vingine vingi vifananavyo na hivyo. Vitu hivi haviwezi kamwe kuleta suluhisho la kiroho katika maisha ya mkristo maana ni vitu vilivyobuniwa kwa akili za wanadamu sio kwa akili za Mungu. Mkristo jifunze na ujiepushe na hizi imani potofu zinazoenea kwa kasi zikionyesha zitafungua malango na milango ya watu wa Mungu kumbe sivyo. Msingi wetu wa wokovu upo katika maneno haya; “Basi, kwakuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili  za wanadamu.” Mdo 17: 29
Pia Mungu ni Roho na wale wanaomwabudu Yeye sharti kumwabudu katika roho na kweli sio kwa mitazamo ya watu wanaopinga maombi na kuwauzia watu vitu vya kiibada za kishetani ili viwalinde. “Basi wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu msijemkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini kaeni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na mwokozi Yesu Kristo, utukufu unayeye sasa na hata milele.” 2Petro 3:17-18
Maana wengi walipotea kwa kufuata uhalifu wa mioyo, maana kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwetu watakavyo kuwepo waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza. Na wengi watafuata ufisadi wao, na wao watajipatia faida ya mali kwa tamaa zao wenyewe wakitumia maneno yaliyotungwa ili kuwanasa yamkini wateule. BWANA anasema, “Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliowekewa.” 2Petro 2:17 
Wapenzi msiamini kila roho bali zijaribuni hizo roho kwamba zimetoka kwa Mungu kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea. Wenye kudanganya wanamfano wa utaua lakini wanazikana nguvu za Mungu. Mkristo usidanganyike hakuna Mungu wa kweli anayepatikana ndani ya chupa bali ndani mwa Maombi. Kristo Yesu alisema waziwazi; “Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” Mathayo 7:7
Ndugu zangu tangu zamani mafuta yalikuwepo lakini hayakutumiwa kiholelaholela kama yanavyotumika sasa, ingekuwa ni hivyo, Yesu Kristo asingewaagiza wanafunzi wake wasiondoke Yerusalemu mpaka wajazwe nguvu za Roho mtakatifu. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Mdo 1:8  Kama mafuta yanaleta upaku au uwepo wa Mungu angeweza kuwapaka mafuta akawaacha waende kutumika, lakini Kristo hakufanya hivyo bali aliwaambia wakae mpaka siku ya Pentekoste (siku ya hamsini baada ya kufufuka kwa Yesu) wakae kwenye maombi. “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto ulio wakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajaalia kutamka.” Mdo 2:1-4

Hivyo tukimwamini Mungu na nguvu zake, yeye anazo nguvu na uweza mkuu wa kugeuza uteka wetu kuwa Baraka. Kila hali unayoipitia iliyo ngumu hata kama ina historia tata kwa Mungu yote yawezekana kwake yeye aaminiye. Simama katika zamu yako geuza uteka. Maandiko yanasema; “Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.” Zaburi  30:11

Nyumba yako ifunike ndani mwa maombi ili isiwe ni nyumba ya misiba, huzuni, umaskini, magonjwa, dhiki na vilio vya uchungu. Bali zigeuza hali zote zisikaribie mlango wako. Usiogope, bali wewe fanya Maombi upate kugeuza, Maana Mkono wake Kristo ni Mkono wenye Nguvu na Uwezo mkuu wa kufungua malango na milango iliyofungwa. Tunajifunza kwa Mfalme Yehoshafati aliwashinda wana wa Moabu na wana wa Amoni kwa Maombi ya kugeuza ubaya wao uwapate wao wenyewe. “Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng’ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi) Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.” 2Nyakati 20:1-3

Wana wa Israeli walipokuwa ndani mwa maombi ya kugeuza uteka; BWANA alilibatilisha shauri la maadui zao. Hata sisi tukiomba kwa uaminifu na kwa juhudi, hakika maadui zetu wa kiroho na kimwili wataanguka mbele yetu. Maana Mungu ni yeye yule jana, leo na hata milele.
“Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka.” 2Nyakati  20:22-24
Katika hili tunajifunza nguvu iliyomo ndani mwa maombi maana tunauona mkono wa BWANA ambavyo unawaangusha maadui wa Israeli walipokuwa kwenye maombi. Tuonapo vita katika ulimwengu wa roho au mwili, hatua ya kwanza ni kumtafuta Mungu aliye hai kwa njia ya maombi. Ndipo maadui zako wataanguka kwa ajili yako. Watu wa Moabu, Amoni na Seiri walipatana kinyume juu ya Israeli lakini BWANA aligeuza shauri lao, panga zao na mikuki yao, ikawachoma wenyewe ili yathibitike maneno ya Mungu yaliyonenwa na kinywa cha nabii Isaya; “Utathibitika katika haki, utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa, na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia. Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. Tazama nimemuumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemuumba mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.” Isaya  54:14-17

Usiogope kwa sababu ya hayo bali yageuze yawageukie wao wenyewe, maana wamechimba shimo lazima watumbukie wao. Geuza kwa Maombi yako na kwa Dhabihu zako. Maana BWANA amekukumbuka tena na atakubarikia tena. BWANA anasema; “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe, usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, usiogope; mimi nitakusaidia.” Isaya  41:10-13
Hakika tukiomba na tukaa ndani mwa maombi; Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.





0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget