Thursday 28 May 2015

SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;

SILAHA YA NANE

UWE MVUMILIVU;

“Uvumilivu” (Greek makrothumia) means patience without reaction (by implication without reaction, long suffering) ikiwa na maana ya ustahimivu; si mwepesi wa hasira wala kukata tamaa. Maandiko matakatifu yanatuelekeza tumwendee BWANA kwa wito wetu. Tukiwa tumejivika uvumulivu. “Kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumulivu, mkichukuliana katika upendo.” Waefeso 4:2

Maisha ya mwanadamu yana mapito mengi sharti avumilie katika BWANA. Pasipo Uvumilivu, hauwezi kupokea jibu toka kwa BWANA kwa kuwa yeye hachelewi wala hawai isipokuwa anajibu kwa wakati wake. Hivyo maisha ya Imani yanahitaji Uvumilivu. “Kwa hiyo ndugu, vumilieni hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza naya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake BWANA kunakaribia. Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la BWANA, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa BWANA ya kwamba BWANA ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape wala kwa mbingu wala kwa nchi, wala kwa kiapo kinginecho chote, bali ndiyo yenu iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.” Yakobo  5:7-12

Mmesikia habari ya uvumulivu wa Ayubu, inasemekana zaidi ya miaka kumi na saba Ayubu alikuwa kwenye hali ya dhiki nzito yenye msiba na magonjwa lakini katika mambo yote hakumkufulu Mungu wala kuwaza kwa upumbavu. Maandiko yanathibitisha; “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.” Ayubu 1:22
Kutokana na uvumilivu basi hivyo BWANA akaubarikia mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake. Akawa na mali mengi kondoo kumi na nne elfu, ngamia elfu sita na jozi ya ng’ombe elfu na punda wake elfu pia BWANA alimbariki Ayubu kwa kumwinulia uzao tena akawa wana waume saba na binti watatu. Wana wa Mungu yatupasa tusizimie roho bali tumtumaini BWANA kwa uvumilivu, “Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki bali njia ya wasio haki itapotea.” Zaburi 1:6

Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Maombi ni lazima yaambatane na Uvumilivu. Bwana anaposema atatenda ni lazima atende kwa wakati. “Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.” Waebrania 10:23

Hivyo Mungu wetu hana kigeugeu, yeye akisema itakuwa lazima iwe tu. Ibrahimu alivumilia miaka ishirini na mitano kabla ya kumpata Isaka kwa Sara mkewe. “Bwana akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. akasema, n’nani  angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.” Mwanzo  21:1-7

BWANA alimpa ahadi lakini ilipita miaka ishirini na mitano ya uvumilivu wa Kiimani. BWANA akageuza huzuni ya Sara kuwa kicheko, akazaliwa Isaka. Nawe Vumilia katika BWANA, Isaka wako atazaliwa pale lango lako  litakapo funguliwa.  “BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwahiyo nafsi imtafutayo.” Maombolezo  3:25

Umkabidhi BWANA njia zako pia umtumaini yeye naye atafanya. Ukae kimya mbele za BWANA nawe umngojee kwa saburi naye atakutendea pale usipozimia roho.

ISAKA naye alivumilia katika BWANA miaka ishirini akiomba kwa ajili ya mke wake Rebeka alikuwa tasa, mwisho wakazaliwa watoto mapacha. Isaka alioa Rebeka akiwa na umri wa miaka arobaini na mke wake alizaa Isaka alipokuwa ametimiza miaka sitini. “Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba, watoto wakashindana tumboni  mwake. Naye akasema, ikiwa ni hivi, kuishi kwa nifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la
pili, na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.” Mwanzo 25:19-26

Yusufu alivumilia mbele za BWANA muda wa miaka kumi na mitatu kabla ya ndoto zake zikatimizwa. “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake, naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari mbaya.” Mwanzo  37:2

Yusufu aliyekuwa na miaka kumi na saba alikuwa akichunga kondoo, akaota ndoto akawajulisha ndugu zake, wakazidi kumchukia wakasema tumuue tuone ndoto zake zitakuwaje. Lengo la ndugu zake Yusufu ilikuwa ni kuua maono na ndoto zisitimie, maadamu mbeba hayo maono alikuwa ni Yusufu ilibidi wapange kumuua na hayo maono. Maandiko yanathibitisha yakisema; “Wakamwona toka mbali na kabla hajawakaribia wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, tazama, Yule bwana ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema mnyama mkali amemla; KISHA TUTONA ZITAKUWAJE NDOTO ZAKE.” Mwanzo 37:18-19

Atukuzwe Mungu asiyeshindwa na jambo lolote, anayetuwazia mema, anayetamka mwisho wetu kabla ya mwanzo. Maana yake kwa imani lazima uuone mwisho wako kabla ya mwanzo ndipo utaweza kuvumilia. Maana; “Mungu si mtu aseme uongo; wala si mwanadamu, ajute; iwapo amesema hatalitenda? Iwapo amenena hatafikiliza?” Hesabu 23:19
Sifa ya Mungu ni thabiti katika kauli zake. Mungu si yule ambaye haaminiki, mwenye kigeugeu au mwenye kubadilika lakini kwa asili yake ni mwaminifu katika ahadi zake na kauli zake. Pamoja na kuuzwa ili ndoto za Yusufu zisitimie, Mungu alimfungulia Milango na Malango baada ya kukaa ndani ya gereza miaka miwili mizima ikiwa inahitimisha miaka kumi na tatu ya kusubilia jibu na wakati wa Mungu kuyatimiza aliyosema kwake. Tunajifunza uvumilivu wa Yusufu na mapito yake maana kila alikopita BWANA alikuwa pamoja naye, ndio maana hata kwa mke wa Potifa alionyesha kumjali Mungu na kumtumainia kuliko ahadi za muda kitambo tu. Akasema; “Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe NIFANYEJE UBAYA HUU MKUBWA NIMKOSE MUNGU?” Mwanzo 39:9
Uaminifu wa Yusufu kwa Mungu ulimfanya ashinde jaribu la kuanguka katika tanzi ya uzinzi na uasherati. Tunajifunza kwa Yusufu alivyokimbia dhambi hii nasi yatupasa kuiga mfano huu kwa kukimbia dhambi ya uzinzi. Dhambi hii imewaangusha wengi na wamepoteza mwelekeo wa kiimani na uwepo wa Mungu. Vijana kwa wazee wanaanguka katika dhambi hii. Na wengi wao wameponzwa na ushawishi wa wenye dhambi kama mke wa Potifa,  badala ya kukimbia kama Yusufu wameingia katika majadiliano mwisho wake wameanguka. “Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.” Mithali 1:10, 15
Baada ya uvumilivu na ushindi wa Yusufu, BWANA alimwinua, tunaona katika maandiko matakatifu jinsi Mungu alivyomkamata Farao kukawa ndio mwanzo wa kuinuliwa Yusufu na wana wa Israeli. “Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri. Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi nyote ya Misri.” Mwanzo 41:41-46

Pia tunajifunza kwa Musa  alipokataa kuitwa mtoto wa binti Farao, alikuwa na umri wa miaka AROBAINI. Lakini alivumilia miaka arobaini akichunga mifugo ya Yethro na akavumilia safari ya miaka arobaini jangwani na wana wa Israeli kuelekea Kanani. Maandiko matakatifu yanathibitisha; “Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akasema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko. Hata miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika mwali wa moto, kijitini. Musa alipouona akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia, Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemka asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri. Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini. Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi, msikieni yeye. Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri, wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui lililompata. Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao. Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika chuo cha manabii, je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka, Miaka arobaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli? Nanyi mlichukua hema ya Moleki, na nyota za mungu wenu Refani, Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu; nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.” Matendo 1:23-43


Pasipo Uvumilivu tutapishana na kalenda ya Mungu, lakini tukivumilia katika BWANA tutavuna mema. “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kishinda, kwa yeye aliyetupenda.” Warumi  8:37

Tutashinda yote tusipovunjika moyo; bali tujinyenyekeze kwa Mungu atatukweza kwa wakati wake. “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.” Zaburi 55:22

DAUDI alivumilia miaka kumi na tatu. Na wakati ulipofika alipokuwa na umri wa miaka thelathini akawa mfalme wa Israeli. Amenusulika kuuawa na Sauli mfalme mara ishirini na tano; lakini Daudi daima aliomba akisema; “Ee Mungu, uniokoe, Ee BWANA, unisaidie hima. Warudishwe nyuma , watahayarishwe, wapendezwao na shari yangu. Warudi nyuma na iwe aibu yao, wanaosema Ewe! Ewe! Washangilie, wakufurahie, wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako waseme daima, Atukuzwe Mungu. Nami ni maskini na mhitaji, Ee Mungu, unijilie kwa haraka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee BWANA, usikawie.” Zaburi  70:1-5

Maombi haya yanafungua Malango na Milango ndani mwa Uvumilivu  wa Kiimani. Mtu mwenye Imani sharti avumilie akidumu katika maombi, maana yuko Jehova aliye hai atasimama. Maandiko matakatifu yanasema; “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.” Ayubu 19:25

Mtetezi wetu hatimaye atasimama juu ya nchi atafuta kila chozi.
“Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima. Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. Wakipita kati ya bonde la Vilio, hulifanya kuwa chemchemi, Naam, mvua ya vuli hulivika Baraka.” Zaburi  84:4-6

Yesu atawalipa watu wake wala hatawaacha bali katika taabu atawatoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi sana lakini BWANA humponya nayo yote.









0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget