Thursday 28 May 2015

SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;

SILAHA YA SABA

UTOAJI WA DHABIHU
Kutoa Dhabihu au Sadaka sio kununua kitu kwa Mungu bali ni ishara ya unyenyekevu mbele za Mungu na ni tendo kamili la Kiibada. Kristo Yesu amefanyika Dhabihu ya dhambi ili sisi tupate ukombozi. Mungu amemtoa Sadaka ili kupitia yeye tufunguliwe mlango na milango ya mbinguni.

Utoaji  wa dhabihu au sadaka ni wa muhimu sana kwake yeye aaminiye maana tangu mwanzo dhabihu zilitolewa. Tunaona hata Adamu na Hawa walipotenda dhambi, BWANA Mungu aliwafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi akawavika. Lakini baada ya Mungu kumwinulia Adamu uzao walizaliwa Kaini na Habili. kutokana na kazi zao walipewa nafasi sawa ya kumtumikia Mungu kwa kazi za mikono yao. Kaini alikuwa mkulima na Habili alikuwa mfugaji. Tunajifunnza kwa watu hawa wawili walikwenda kumtolea Bwana Mungu dhabihu (sadaka ya hiari) mbele za BWANA. Maandiko yanathibitisha; “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabari Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akagadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, kwanini unaghadhabu? Na kwanini uso wako umekunjamana?. KAMA UKITENDA VEMA, HUTAPATA KIBALI? Usipotenda vema dhambi iko inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwanzo 4:3-6
Mungu alimuumba mwanadamu kwa ajili yake. Ili amwabudu yeye, awe furaha yake iko nafasi moja tu katika moyo wa mwanadamu ya ibada. Na hii ni kwa ajili ya Mungu pekee. Mungu ni mwenye wivu asiyetaka kamwe kuchanganywa na miungu mingine. Ndiyo maana Mungu aliweka amri katika amri kumi “Mimi ni Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa usiwe na miungu mingine ila mimi.” Kutoka 20:1-2

Suala la kumwabudu Mungu linaambatana na kumtolea Mungu sadaka. Sadaka za wana wa Adamu, Kaini na Habili inaonyesha kielelezo cha kumkaribia Mungu kwa ibada. Tendo la kukubaliwa sadaka ya Habili ni kielelezo cha kukubaliwa mtoa sadaka. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Kaini akamgadhibikia ndugu yake kwa sababu Mungu alizikataa sadaka za Kaini kwa sababu moyo wake haukuwa mkamilifu. Maana BWANA anasema, “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA bali maombi ya mtu mnyoofu ni furaha. Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA. Bali humpenda mtu afuatie wema.” Mithali 15:8-9

Ndiyo maana hoja ya Mungu kwa Kaini inasema; KAMA UKITENDA VEMA, HUTAPATA KIBALI? (If you do what is right, will you not be accepted?) Ili mtu wa Mungu dhabihu yake ikubalike mbele za Mungu sharti awe na moyo mnyoofu. Habili anatajwa na maandiko matakatifu ya kuwa ni shujaa wa imani aliyetoa sadaka iliyo bora ambayo inanena mbele za Mungu. “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo ijapo amekufa angali akinena.” Waebrania 11:4
Mungu aliikubali dhabihu ya Habili kwa sababu alikuwa mwenye haki na mtiifu. Nuhu alipokwisha kuokolewa na Mungu yeye na jamaa yake toka kwenye gharika tunaona anamjengea BWANA madhabahu na kutoa dhabihu. “Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, sitalaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.” Mwanzo 8:20-21

Baada ya kuokolewa lazima tumkaribie Mungu kwa maombi na sadaka. Tunajifunza katika utumishi wa Nuhu wa utoaji sadaka uliosababisha BWANA atoe tamko la kutokuangamiza tena baada ya kusikia harufu nzuri ya sadaka nzuri zilizotolewa na Nuhu. Kwa sadaka waweza kuikoa familia yako na maangamizi ufanyavyo hivyo ndani mwa maombi. Mungu hakutoa tamko la kutokuangamiza tena kabla ya sadaka bali ni baada ya sadaka kutolewa. Hivyo Mungu akambarikia Nuhu na wanae. Na akafanya agano nao la kutofuta kizazi chao tena kwa gharika. “Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya ghalika; wala hakutakuwa tena ghalika, baada ya hayo kuiharibu nchi.” Mwanzo 9:11

Tunajifunza pia kwa Ibrahimu baba yetu wa imani alimwabudu Mungu katika roho na kweli na kutoa dhabihu juu ya madhababu. “BWANA akamtokea Abram, akasema, uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhababu BWANA aliyemtokea. Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhababhu huko, kaliitia jina la BWANA.” Mwanzo 12:7-8

Ibrahimu aliitwa rafiki wa Mungu kwa sababu alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora, hata alipokuwa amepewa mtoto Isaka, alipotakiwa kumtoa mwanawe mpendwa wa pekee aliyempata katika uzee hakumzuilia Mungu. Tunasoma hivyo katika maandiko matakatifu “… Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko katika mlima mmoja wapo nitakao kwambia… wakafika mahali pale walipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhababu huko akaziweka tayari kuni kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe… kwa maana sasa najua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee… kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwano, mwanao wapekee, katika kukubariki nitakubariki, na katika kukuzidisha nitakuzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao na katika uzao wako mataifa yote duniani watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.” Mwanzo 22:1-18

Kwa tendo hili Ibrahimu alihesabiwa kuwa mwenye haki pale alipomtoa mwanawe juu ya madhabahu. Imani ya Ibrahimu ilijidhihirisha katika utii wa kweli kwa Mungu. Yeyote atakaye kutembea na Mungu kwa karibu yampasa kuwa tayari kumtoa “Isaka” wake madhabahuni. Ibrahim aliitwa rafiki wa Mungu kwa sababu ya kukubali kutoa Isaka wake. Wakristo wengi wanatoa ili mradi wanatoa, hawatoi kilicho bora bali wanatoa bora sadaka. Lakini tujifunze kwa watu hawa wawili Habili na Ibrahimu tunaona utoaji wao ni utoaji ulio bora, walitoa sadaka zinazowagusa wao wenyewe, maana Isaka anatolewa mzima-mzima madhabahuni pa BWANA. Hivyo hakuna kuabudu kuliko kamili kusiko ambatana na utoaji. Kila mtu katika biblia aliyetoa sadaka bora ilidhihirisha ubora wa maisha ya mcha Mungu. Maandiko yanathibitisha katika kitabu cha 1Nyakati “Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, leteni sadaka mje mbele zake; mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.” 1Nyakati 16:29
Kipindi hiki cha nabii Eliya mtishibi alipotaka kukomesha imani potofu za miungu katika Taifa la Israeli, zilizoanzishwa na mfalme Ahabu mwana wa Omri na mke wake Yezebeli binti Ethbaali mfalme Wasidoni. Mfalme huyu na mke wake walimjengea Baali madhabahu huko Samaria na wakamsujudia. Katika biblia mfalme Ahabu anahesabika kuwa mfalme mwovu sana miongoni mwa wafalme wa Israeli. BWANA alipokuwa amemwinua Eliya mtishibi kipindi hiki Ahabu alikuwa amewaua manabii wengi mno wa Mungu aliye hai. Ilibidi afanye maombi ya kufunga malango na milango juu ya Israeli, akaifunga mvua isinyeshe katika nchi miaka mitatu na nusu (3½) maandiko yanasema; “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja nasisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu yanchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda.” Yakobo 5:17-18
Maombi ya mwenye haki sharti yaambatane na kutoa dhabihu mbele za Mungu aliye hai, tunajifunza kwa Eliya nabii.“Kisha Eliya akamwambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhahabu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata-kata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema fanyeni mara ya pili, wakafanya mara ya pili. Akasema fanyeni mara ya tatu, wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu, akaujaza mfereji maji. Ikawa wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wew umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja, wakawakamata, na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.” 1Wafalme  18:30-46

Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; tunajifunza tendo la imani kwa mtumishi wa Mungu nabii Eliya jinsi alivyobeba watu wake kwa kabila zao na kuwainua mbele za BWANA kwa njia ya maombi, kisha akazipanga zile kuni, akamkata-kata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Tunajifunza kuwa maombi na dhabihu vinakwenda pamoja madhabahuni pa BWANA. Ikawa wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu.

Moto wa BWANA unawakilisha uwepo wa Mungu na nguvu zake. Maombi haya ya kufungua Malango na Milango sharti yaambatane na Kutoa Dhabihu mbele za Mungu aliye hai. Eliya Mtishibi ili akomeshe taabu, dhiki na mateso kwa Israeli vilivyotekwa na mfalme Ahabu na mkewe Yezebeli kwa kuungamanisha taifa kwa miungu ya Wasidoni mungu aitwaye Baari na Ashtoleth; Eliya alisimama mahali palipo bomoka, akajenga Madhabahu ya BWANA tena iliyokuwa imevunjika. Kwa mawe kumi na mawili sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli.

Hata Mungu mwenyewe, ili amwokoe mwanadamu na dhambi, alimtoa mwanawe wa pekee Yesu kristo, ili awe kuhani mkuu atakaye wapatanisha kwa njia ya kifo cha msalaba. Ili kwa damu yake Kristo Yesu wanadamu wapate ukombozi maana pasipo damu hakuna ondoleo la dhambi. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana  3:16

Vitu vyote tulivyo navyo vyatoka kwake na viko kwa uweza wake, hivyo tunapotoa Dhabihu zetu mbele zake yeye Mungu aliye hai ni tendo la Kiimani la Kujiungamanisha naye kwa neno na kwa tendo.
“Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena? Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.” Warumi  11:35-36

Maombi yetu ya kufungua malango sharti yatubebe Sisi, Watoto wetu na Mali zetu. “Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni, Mioyo yetu na mikono.” Maombolezo  3:41

Maana yake; Wewe binafsi ufunguliwe Malango na Milango, Watoto wako wafunguliwe Malango na Milango, Mali zako, Kazi yako, Biashara yako, Elimu yako na Vyote Uvitendavyo vistawishwe katika BWANA visizae Kufa-kufa wala Mapooza. “Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote, Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.” Mithali  3:9-10


Bwana yeye ndiye atupaye Baraka na Ustawi si vinginevyo, Lazima tujinyenyekeze kwa Maombi yeu na Sadaka zetu zilizo bora. “Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, UTAJIRI na HESHIMA katika mkono wake wa kushoto. NJIA zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana, Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.” Mithali  3:16-18

Baraka za Mungu zipo kwao waliotayari kuzifuata na kushikamana nazo. Unapo mwomba Mungu na kutoa Dhabihu zako Madhabahuni pake, Yeye hushuka kwa nguvu zake na atakupa Baraka zifuatazo:-

(i) WINGI WA SIKU; maana yake Maisha marefu.
      BWANA anasema; “Utafika kaburini  mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.” Ayubu  5:26

(ii) UTAJIRI na HESHIMA;
     Vinaambatana na USTAWI katika kazi yako yote ya mikono. “Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.” Mithali  8:20-21

Jambo la msingi lazima kila mmoja wetu anayeitwa kwa jina la BWANA, sharti ajenge Madhabahu ya BWANA kwa ajili yake na familia yake. Maana yake ni Kumrejesha Mungu wa kweli katika familia. Panahitajika mtu atakaye batilisha hiyo miungu ya ukoo, miungu ya kichifu, isitende kazi kwa kuivua madhabahuni kwa njia ya maombi na dhabihu ili maandiko yatimie ya Mtunga Zaburi. “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.” Zaburi  20:7-8
Baada ya kuokoka na kuvishwa uwezo wa ki-Mungu kwa njia ya imani yatupasa kuchukua hatua za kiimani ndani mwa maombi ili KUBATILISHA na KUTENGUA ibada za miungu na matoleo yake (makafara), yaliyotolewa kabla. Ibada za miungu hufanyika kwa njia ya maombi na dhabihu japo hazitolewi kwa mungu wa kweli lakini mfumo unaweza kufanana na wa ibada za kweli, ndiyo maana manabii wa Baali walijenga madhabahu na kutoa sadaka. Tunaona katika maandiko; “Eliya akawaambia manabii wa Baali, jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeneza kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu wal msitie moto chini… wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri wakisema Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliye jibu. Nao wakrukaruka juu ya madhabahu aliyoifanya… ikawa wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.” 1Wafalme 18:25-29 

Tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Ayubu jinsi alivyoomba na kutoa dhabihu kwa Mungu aliye hai; Ayubu alikuwa anawaombea daima watoto wake na kuwatolea dhabihu mbele za BWANA, kila mmoja alimtolea Maombi na Sadaka. Hata Shetani alipowatamani watoto wa Ayubu na akatamani kumfilisi Ayubu, alishindwa mpaka alipomwendea Mungu kuomba apewe ruhusa.

Maisha ya Ayubu na familia yake yalijulikana daima mbele za BWANA. Tunasoma katika maandiko matakatifu yanasema; “Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi namapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote. Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake umeiongezeka katika nchi.” Ayubu 1:5-10

Ayubu hakuwaacha watoto wake nyuma katika Ibada, bali aliwabeba daima na kuwaombea. Mungu alimzingira pande zote yeye na familia yake pamoja na mali zake zote, BWANA aliwawekea UKINGO, shetani akashindwa kuwanasa.

Tunapata siri ya ki-Mungu ya kwamba tumwombapo Mungu na kutoa dhabihu zinazokubalika mbele zake, Yeye hutuwekea ukingo pande zote. Ukingo maana yake ni ukuta, boma, ngome, jabali, mwamba. Na BWANA anasema; “Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.” Zekaria 2:5

Lazima uchukue hatua ya Kiimani kumwendea Mungu Madhabahuni pake. Omba, Ombea, Watiishe watoto wako kwenye Maombi na Sadaka popote walipo na adui hatawanasa kamwe. “Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake umeiongeza katika nchi.” Ayubu  1:10

Inua Biashara yako mbele za BWANA, Inua kazi yako mbele za BWANA, Inua Elimu yako mbele za BWANA kwa maombi na sadaka. “Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Leteni sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.” 1 Mambo ya nyakati  16:29

Leteni Sadaka, mje mbele zake, Inua mikono mje mbele zake kwa Maombi ili BWANA aweke Ukingo kwako, Mabaya yasikupate na Ulinzi wake ukufunike.

Tunaona mtumishi wa Mungu mfalme Daudi alipokuwa na msiba uliotokana na pigo la ugonjwa wa tauni toka kwa BWANA. Maelfu ya watu yamekwishakufa katika nchi yake, wakati Daudi hajui cha kufanya ili kuondoa mauti juu ya nchi ndipo anaambiwa na Mungu ajenge Madhabahu na atoe Dhabihu. “Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia, Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake, tazama ng’ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe, viko kwa kuni. Vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake, wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizo zigharamia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekel hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliidhiria nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.” 2 Samweli  24:18-25

Tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Daudi jinsi alivyotoa Sadaka yenye gharama na bora aliyo gharamikia yeye mwenyewe. Matokeo yake tunayaona baada ya Daudi kutoa dhabihu kifo kilizuiliwa kwa watu wake. Tukio hili ni la kiimani na la kuigwa kwa watu wa Mungu. Tunayaona Maombi ya kufungua Malango na Milango ni sharti tumwendee Mungu madhabahuni, Tumjengee madhabahu na Tutoe Sadaka; naye atashuka Kuzuia Magonjwa, Mateso, Misiba na kila aina ya Vifungo. Hivyo Usiogope; Jenga Madhabau yako, Toa Sadaka, hayo yaliyokupata yataondolewa na kuzuiliwa yasije kwako tena. Dhabihu yako, Igeuze Msiba wako kuwa Uzima, na kwa wale unao waombea na kuwainua mbele za Mungu aliye hai.

“Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.” Zaburi  50:23

Lazima nasi tunapofunguliwa Malango na Milango; fahamu wako wengi watupingao watatufuata-fuata  kwa ubaya, Nawe usimamapo katika maombi nyosha mkono wako juu yao, kinyume, warudishie mabaya yao, yawalambe, wavishwe fedheha yao. “Bwana akamwambia Musa, nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao Wasmisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.” Kutoka 14:26-28

Usiudharau Mkono wako, Musa aliponyoosha mkono wake juu ya bahari, BWANA alifungua njia na mlango kwa wana wa Israel wakapita, Bahari ikawa nchi kavu. Nasi tukinyosha mikono yetu kwa Jina la Yesu Kristo yatafanyika na Malango yatafunguka. “Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.” Mithali  5:22



0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget